Sunday, February 12, 2012

MUME MWEMA

Neno la leo linatoka: 1Petro 3:7
“Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa AKILI; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe”
TAFAKARI:
Kwa asilimia kubwa matatizo yanayotokea katika ndoa chanzo chake ni mwanaume kutojua kuishi kwa akili na Mke wake. Ni kweli kuna wanawake wajinga ambao biblia inasema wanavunja nyumba zao kwa mikono yao wenyewe, pamoja na hayo kama mwanaume ataomba Mungu ampatie Hekima au akili Ndoa inadumu. Kumbuka kila unalotenda kwa mwenzio linazaa tendo la kutendewa likiwa baya au jema. Tatizo likitokea katika ndoa, kaeni chini mtafute chanzo cha tatizo, Mume ana sehemu ya kutumia akili aliyopewa na Mungu kurudisha mahusiano. Hebu tuangalie baadhi tu ya mambo anayotakiwa mwanaume kumtendea mkewe:

MUME AMHESHIMU MKE WAKE: Kuna wanaume wanadharau wake zao, utakuta mke anatukanwa, kupigwa, anakosolewa mbele ya watoto au hata mbele ya watu kama house girl. Mara ngapi tunasikia wanaume wakigomba “Mama Fulani chakula gani hiki mbona ugali haujaiva vizuri?”, lawama hizo mbele za watu au mabinti wa kazi – ni kumuaibisha mkeo, na kwake ni tatizo kubwa. Mke ni tofauti kabisa na watoto au wasichana wa kazi, anatakiwa kupewa Heshima, huyo ni mwenzi wako na mshauri wako. Kufanya Mapenzi na wanawake wengine ni kumdhalilisha mkeo na kwa sababu mapenzi hayagawanyiki lazima matatizo yataanza.

MUME AMJALI NA KUONYESHA UPENDO KWA MKE: Mwanamke ana hisia kali za mahusiano, anabadilika kulingana na anavyotendewa, wakati mwingine wanakuwa kama watoto, unaweza kumdanganya hata kwa kitu kidogo ili mradi kiashirie kumpenda. Siku moja jaribu kununua Pipi, halafu mwambie “sweet” au “Darling” nimekuletea zawadi kubwa, twende nikakupe chumbani, halafu toa pipi huku ukimtazama usoni, utashangaa yatayotokea. Onyesha kuwa unamjali, unamthamini, unampenda na unafurahia ukiwa nae. Hata kama ana kazi yake, Mnunulie nguo rasmi kama zawadi. Neno Pole Mpenzi, Samahani, Umependeza n.k. yana maana sana kwa Mwanamke. Mume awe na muda wa kuongea na Mke wake, kushinda kwenye Mabaa hadi usiku, kuwa busy na TV au Kompyuta muda wa usiku ni tatizo kwa mwanamke. Wanaume wengi wanacheka na kupiga porojo na wanawake wengine maofisini, lakini akifika nyumbani utafikiri ameambiwa yuko mahakamani penye amri ya usipige kelele.  

MUME NI KICHWA CHA NYUMBA: Tangia mwamzo Majukumu ya kutunza familia ni ya Baba, mwanamke ni msaidizi, siku hizi mambo yamegeuka, akina mama ndio wanaachiwa mizigo ya kulea familia, Mke akiwa na kazi au biashara ndio usiseme, Nguo za watoto, chakula, ada n.k. yote anaachiwa Mama. Baba hakikisha unaacha fedha za kutosha nyumbani, wengi wanapenda chakula kizuri huku wanaacha fedha za fungu moja la mchicha, na wengine wanakula vizuri wakiwa kazini – Supu, Biliani, Pilau mbuzi, Juice – familia nyumbani ni maharage wakibadilisha Mchicha.

MPATIE HAKI YAKE YA NDOA: Ni wajibu wa Mume kumtimizia mkewe hitaji la Ndoa, jambo hili siku hizi limekuwa tatizo kubwa. Wanaume wengi WANABAKA wake zao, kwa maneno rahisi ni kwamba wanafanya tendo la ndoa kutimiza wajibu sio kwa ajili kupeana mapenzi. Utakuta mwanaume anaparamia tu wala hakuna maandalizi, siku nzima wameshinda hawaongei, usiku ukifika ni Amri za Jeshi “SIMAMA JUU, KULIAAAA GEUKA, MGUU PANDE, MWILI LEGEZA” hizo kwa mwanamke ni Karaha au Adha badala ya Raha. Wanaume wengi ni wabinafsi katika swala hilo, wanajali kutimiza haja zao, kuna akina mama hawajawahi kufikishwa mwisho wa Raha, japo kila siku wanatoa huduma. Hili jambo linahitaji elimu ili kila mmoja aone furaha ya Ndoa. Kwa tatizo la kiafya, nitalitolea maelezo katika somo lijalo, hakuna haja ya kuwatajilisha wamasai kwa dawa zao za kutunza heshima ya Ndoa.

MUNGU ABARIKI NDOA ZETU ZIWE NA MWANZO MPYA WENYE FURAHA NA AMANI TELE

Ev:  Eliezer Mwangosi.
0755808077 & 0652571733

UPENDO NA UTII KATI YA WANANDOA

Neno la leo linatoka:  Waefeso 5:25
“Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake”
tAFAKARI:
Mara nyingi wanandoa wanapofarakana utasikia Mume anasema mke wake hamtii, na mwanamke anadai mume wake hampendi, sasa nani anatakiwa kuanza? Kutii au kupenda! Kabla sijaanza kuongea juu ya sifa za Mume mwema, nitaanza kueleza falsafa ya Maneno haya mawili “Kupenda na Kutii” yanavyohitaka kutumika katika Ndoa.

UPENDO WA MWANAUME: Upendo wa kweli kwa mwanaume juu ya mke wake, ni ule tu unaojengwa na Mungu, wengine wanasema, hauna sababu, ndio maana utakuta watu wanaulizana hivi huyu mume amempendea nini?. Adam alipatiwa mke na Mungu, alichukuwa ubavu wake akamfanya Hawa, alipopelekewa AKAMPENDA. Hivyo upendo wa kweli wa Mume kwa Mke wake, huanzishwa na Mungu, ndiyo maana Paulo anamfananisha Mwanaume, kama Kristo alivyolipenda Kanisa. Wanaume wengi siku hizi hawapendi ila wanatamani au kupenda vitu Fulani. Mfano: Wengine wanapenda Makalio bila kujua kuna ya Mchina, wengine “Figure eight”, wengine Maziwa yaliyosimama – mama akianza kunyonyesha Upendo kwisha, upendo wa namna hiyo ni wa kitambo, ndoa nyingi zinaanza na upendo huo, baada ya muda mfupi Ndoa inakuwa Karaha.

UTII WA MWANAMKE: Watu wengi kwa kutokuwa na elimu ya Biblia, wametafsiri neno hili vibaya hasa wanaume. Ukisoma biblia ya lugha ya Kiingereza na lugha zingine za asili ya waandishi wa Biblia, utii wa mke kwa mume ni tofauti na utii wa Mtoto kwa wazazi au watumishi kwa Bwana zao. Utii wa Mke kwa Mume unaitwa “SUBMIT” wakati Utii wa Mtoto au watumishi unaitwa “OBEY”. Soma biblia ya kiingereza – KJV “Waefeso 5:22, 6:1, 6:5”. Wives are supposed to SUBMIT themselves to their Husbands, while children are supposed to OBEY to their parents. Mwanamke anatakiwa KUJISALIMISHA kwa Mumewe kwa UPENDO akiamini juu ya UPENDO  wa mume wake, anakubali kuwa ubavu au msaidizi wa mumewe. Wanakuwa mwili mmoja. Ukiona mwanamke kawekewa Sheria nyumbani na anatakiwa kutii kama mtoto, huo sio mpango wa Mungu, na ndoa lazima itaishia kuwa Jela Ndogo – Jambo hili ni pan asana linahitaji hekima ya Mungu kulielewa na kulitenda.

Ukielewa falsafa hiyo, mwanaume hatadai mwanamke amtii kwanza ndipo ampende, Mungu angefanya hivyo, Kristo asingekuja kutukomboa tungali wenye dhambi, alitupenda tungali wabaya. MUME MPENDE MKEO, MLEJEZE KWA UPENDO KAMA KRISTO ANAVYOTUNDEA.

MUNGU AWAPATIE SIKU NJEMA YENYE FURAHA AMANI NA BARAKA TELE

Ev:  Eliezer Mwangosi.
0755808077 & 0652571733

MKE MWEMA

NENO LA LEO LINATOKA:  Mithali 14:1
“Kila mwanamke aliye na Hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu hibomoa kwa mikono yake mwenyewe”
TAFAKARI:
Kuna mithali isemayo “MAJUTO MJUKUU”, ni kawaida kwa wanandoa kuangalia na kulaumiana juu ya matatizo yanayojitokeza, badala ya kutafakari chanzo cha matatizo. Matatizo mengi ya ndoa yanatokana na wanandoa kutokuwa na elimu ya ndoa na kutofuata ushauri wa Mungu aliyeanzisha Ndoa. Baadhi ya sifa za Mwanamke mwenye Hekima – Pia Soma Mithali 31:10-31.

1.     Hufumbua kinywa chake kwa hekima, Na sheria ya wema I katika ulimi wake (31:26). Wanawake wengi hawajui kuutumia ulimi vizuri – Ukali, maneno ya mikato, matusi, ukaidi n.k. kwao ni mambo ya kawaida. Wengi wanatawaliwa na HASIRA na WIVU, akiona mumewe anacheka na mwanamke ni Kosa la jinai, mwanamke anafura wala hata hawezi kuongea, hali ya hewa inabadilika hata paka nyumbani wanatambua kuwa hali ni Mbaya.

2.     Hufanya kazi kwa Moyo na Huamka alfajiri na mapema
Kuna wanawake ambao ni wavivu kupindukia, inafika wakati hata kutandika kitanda anamtuma House Girl, wanaume ni rahisi sana kuvutwa na anayemhudumia kwa ukaribu, House girl akiandaa chakula, mara kitanda, mara maji ya kuoga, mara apige deki chumbani n.k. Haichelewi mwanaume kulipa fadhila kwa wema anaotendewa.

3.     Ni msafi na anajua kuandaa mavazi yanayofaa kwa familia yake
Kuna wanawake ambao ni wachafu – usishangae kukuta sufuria kwenye makochi, chumba cha kulala ni stoo ya nepi za mikojo na nguo chafu, wengine kuoga ni anasa. Mwanamke ni MAJI, sharti mwanamke awe msafi muda wote. Wanaume wote wanapenda Usafi, marashi hata ya mchina yasikose, Mwanamke hakikisha “Reception” inakuwa Safi na kuwa katika hali ya kumfanya Mume ajisikie kujipumzisha kwa Raha mstarehe.

4.     Jali na timiza Mahitaji ya NDOA kwa mume wako
Sulemani anasema mwanamke mwema “Taa yake haizimiki usiku”, kuna wanawake wavivu kwa swala hili, pia kuna wanaopenda kulipa visasi kwa kuwanyima waume zao huduma, utakuta wiki nzima mama apanda kitandani huku amevaa “KOMBATI” utafikiri ni askari anaenda vitani. Wanaume ni sawa na Mbuzi ambao hawachelewi kukata kamba wakikosa majani walipofungiwa. Fanya makosa yote, lakini usijefanya ujinga wa kumkomoa mume kwa kumnyima huduma ya Ndoa, hilo ni kosa la Jinai. Hakikisha huduma hizo zinaboreshwa, nenda na wakati ili mradi isiwe kinyume na taratibu za Mungu.

5.     Mwanamke anatakiwa kujua kupika chakula kitamu, ambacho familia itafurahia.
Wanawake wengi hasa wa siku hizi hawajui kupika, ndio maana utakuta wanaume wengi wanaishia kula hotelini au kwa mama ntilie, kama umetoka bara basi usione aibu kujifunza kwa watu wa pwani namna ya kuunga NAZI kwenye chakula. Akina mama ni wajibu wao kujifunza Mapishi, Mchicha peke yake unaweza kuwa na mapishi zaidi ya 10, wanaume wanapenda chakula chenye ladha “Test”, mfanye mume akumbuke chakula cha nyumbani.

6.     Mwamini Mume wako, wivu na hisia mbaya ni adui wa ndoa yako. Usitoe siri za ndoa yenu kwa mashoga au ndugu zako. Muda wote muombe Mungu akupatie hekima ya kuongea pindi tatizo linapotokea, Muombee mume wako ili Mungu amsaidie pia awe na Hekima ya kutunza Ndoa kwa Uadilifu na Upendo.  

Mungu awajalie hekima katika maisha ya Ndoa ili Furaha, Amani na Upendo vipate kudumu daima.

Ev:  Eliezer Mwangosi.
0755808077 & 0652571733