Thursday, December 29, 2011

MALEZI YA WATOTO

UJUMBE WA LEO:  Mithali 22:6
“Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee”
tAFAKARI:
Kuna visa vingi tunavishuhudia juu ya tabia za Watoto wa kizazi cha leo, siku moja tulikuta mwalimu anaendesha Kesi kati ya Mtoto wa kiume wa darasa la tatu aliyekuwa amembaka mtoto wa kike. Alivyoulizwa mambo hayo ameyajulia wapi, akadai alifundishwa na Dada yake mlezi (House Girl). Kumbe tangia alipokuwa mtoto mdogo House Girl alikuwa akimfanyia mchezo wa kukidhi haja yake ya Ngono. Wazazi wengi wanalia juu ya tabia za watoto wao kuharibika, mara nyingi tunasikia “Heri kutozaa kuliko kuzaa mtoto wa tabia hii” Kama watoto wako hivyo! unategemea kuwa na Vijana wa namna Gani na hatimaye wazee wa namna gani?.

Kulingana na mfumo wa maisha tunaoishi, ni ndoto za mwenda wazimu kuwa na Jamii yenye maadili kwa sababu:
1.    Wazazi hawana Muda na watoto wao, Mfanyakazi ndiye mlezi, hivyo watoto wanarithi tabia ya House girls. Mama na Baba hawana muda wa kukaa na watoto, sanasana weekend, nazo utakuta kila mtu yuko busy na shughuli za nyumbani.
2.    Walezi wengine wa watoto ni TV, watoto wanaharibika kwa sababu, muda mwingi wako huru kuangalia TV, kwa sababu wazazi muda mwingi hawako nyumbani. Na zaidi utakuta Mdada wa kazi yuko huru kujiwekea Picha zozote, ambazo athari yake ni kubwa kwake mwenyewe na watoto.
3.    Wazazi wengi wa siku hizi hawako makini na mambo wanayoyafanya mbele za watoto. Watoto wengi utaona wanafanya  mchezo wa Baba na Mama, Baba juu na Mama chini, wanaona wapi? Kama sio mtindo wa kulala na vitoto, utafikiri watoto wamelala kumbe wanasikilizia, huku wakiinua shuka kuchungulia. Wengine vyumba vyao havina Siri, chumba cha pili kikiwa cha watoto, Faragha ikianza tu, watoto chumba cha pili ni shida tupu, unafikiri hao watoto au vijana kesho watafanya nini?
4.    Watoto hawapati Muda mzuri wa kujifunza neno la Mungu, ambalo ndilo linaweza kuwahekimisha. Neno la Mungu linasema “Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, bali Wapumbavu hudharau hekima na Adabu” Mithali 1:7.

Wapendwa, pamoja na Maisha haya, tunawajibika kulea watoto, Mtoto anatakiwa kurihi tabia ya Mama, Ndiye mwalimu wake mkuu, Akili ya mtoto inakuwa tupu anapozaliwa, anategemea akili ijazwe na mambo anayosikia na anayoona kila mara. Je Mtoto wako akili yake inajazwa na Maneno na Matendo ya NANI? Hiyo ndiyo tabia yake ya Baadaye. Matusi na Maneno yasiofaa hayatakiwi mbele za watoto.

MUNGU ABARIKI FAMILIA ZETU NA KUTUPATIA BUSARA ZA NAMNA YA KULEA KWA AJILI YA MAFANIKIO YA BAADAYE 

Ev:  Eliezer Mwangosi

NDOA IHESHIMIWE

Ujumbe wa Leo unatoka:  Ebrania 13:4 
Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu”
TAFAKARI:
Kama kuna bidhaa adimu katika maisha ya siku hizi, ni HESHIMA KATIKA NDOA. Wana ndoa asilimia kubwa hawaheshimiani, lakini pia hata watu wa nje hawaheshimu Ndoa za wenzao.

Utasikia matusi ya nguoni yakirushwa kati ya wanandoa mbele za watoto, magomvi ya usiku yasiyokoma, kunyanyasana, dharau, maneno ya mikato, kununiana n.k. yote hayo ni kukosa heshima katika ndoa.

Mawifi, mashemeji, akina mama mkwe n.k. tunashuhudia wakianzisha tafrani katika ndoa za ndugu zao. Bila kuwasahau wanaowasha mapenzi kwa waume au wake za watu. Hayo yote ni kuvunja heshima ya ndoa. Mithali 5:15 inasema “Unywe maji ya Birika lako Mwenyewe”. Uliona wapi watu wanapokezana vijiko wakati wa kula? Huo sio ustaarabu na kukosa HESHIMA.

Sehemu nyingine inayopaswa heshima ni chumbani, sehemu pekee ya kupumzisha akili na kupata furaha ni wakati wa faragha. Wapendwa leo kuna kesi nyingi na matatizo mengi ya wanandoa, hata magonjwa, yanayotokana hapo chumbani. Wengi vyumba vyao vimegeuka kuwa KARAHA, ni amri kama jeshini, ndio maana hata madereva wa magari wanalazimika kwenda Shule, angalia madereva taxi wengi wako “very rough” na gari zao hazidumu.
Pia sharti wanandoa wakumbuke kuwa kila kiungo cha mwili kiliumbwa kwa kazi maalumu, ndio maana hatujawahi kuona wanyama wanafanya tendo la ndoa kinyume na maumbile, mambo hayo athari zake ni kubwa. Hebu, UPENDO NA AMANI vitawale katika viwanja vya FARAGHA.

NAWATAKIA SIKU NJEMA YENYE AMANI NA MAFANIKIO TELE

Na: Eliezer Mwangosi

HASIRA HASARA - KATIKA NDOA

Ujumbe unatoka:  Waefeso 4:16 
Muwe na HASIRA, ila msitende dhambi; Jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka”
TAFAKARI:
Asilimia kubwa ya NDOA za siku hizi hazina AMANI, utasikia mama anasema heri nisingeolewa, na wakati mwingine Baba anafikiri alikosea, huenda huyo mwanamke halikuwa chaguo sahihi. Wanasahau kuwa wakati wa uchumba na hatimaye “honey moon” (Fungate), walikuwa wakipakatana wakilishana na kunyweshana Juice. Lakini leo watu wanalala huku wanaomba usiku uishe haraka.

Leo tunatafakari juu ya HASIRA na Kuwa na machungu moyoni, Kuna watu wanahasira za Kijinga, utakuta mtu amefura hawezi hata kuongea. Lakini ukifuatilia utakuta KOSA ni dogo, mfano: Mwanamke anamuona mume wake anacheka na mdada anayefanya naye kazi. Moja kwa moja wazo linamtuma kuwa anaibiwa, Mara mama anaanza kununa, inafika usiku Mama anapanda kitandani na NGUO utafikiri ameambiwa ajiandae kukimbiza mwizi usiku. Na mwanaume akiona adhabu inazidi, siku ya kwanza, ya pili, ya tatu, wiki - anaanza kuzungusha macho barabarani utafikiri “WIPER” za Isuzu. Unashangaa Mama anaanza kuvaa kanga za Mafumbo “Utazunguka kila Bucha Nyama ni ileile” na utakuta Baba wala hana habari ya Kusoma maneno ya Kanga. Mwisho wa yote NDOA inaishia kuwa Jera ndogo ambayo, Upendo, Furaha na Amani vinabaki kuwa historia.

Wapendwa, hasa wenye ndoa changa, jueni kuwa, Ndoa ni Muungano wa watu wawili waliodhaifu, walioazimia kuishi wakichukuliana na kusaidiana. Tatizo sio kukosewa au kukwazwa, shida kubwa ni namna ya kuchukuliana hasa mwenzio anapokukosea. Kumbuka mwanadamu yeyote sio mkamilifu “SIO MALAIKA”, hivyo kukoseana lazima kutatokea, na SHETANI anaitumia hali ya kukoseana vizuri, atakuletea hisia mbaya na kukujaza hasira na Machungu Moyoni ambayo madhara yake ni SUMU YA NDOA. Katika hali zozote unapoona umekosewa, omba hekima kwa MUNGU atakupatia njia nzuri ya kulitatua tatizo kwa AMANI, waswahili walisema “HASIRA - HASARA”. Mungu anasema "Hasira hukaa kufuani mwa wapumbavu" Mhubiri 7:9

MUNGU ATAWALE NDOA NA FAMILIA ZETU – NAWATAKIA SIKU NJEMA

Ev. Eliezer Mwangosi

ADUI WA NDOA YAKO

UJUMBE UNATOKA:  Warumi 16:19-20
“Maana UTII wenu umewafikilia watu wote; basi nafurahi kwa ajili yenu, lakini nataka ninyi kuwa wenye HEKIMA katika mambo MEMA, na wajinga katika mambo mabaya. NAYE MUNGU WA AMANI ATAMSETA SHETANI CHINI YA MIGUU YENU UPESI…..”
AFAKARI:
Baada ya kufanya uchunguzi, imebainika kuwa kadri tunavyoendelea kuishi, kati ya ndoa 100, ndoa 95 zinapitia changamoto za Migogoro ambayo mwisho wake ni kuachana, na hata kama hawajapeana talaka, basi wanaishi kwa matumaini. Yaani wanaomba lolote litokee ili waondokane na Adha ya maisha ya Ndoa. Utakuta watu wanatembea Barabarani wanaongea peke yao, au wanafika maofisini wakiwa na MALUWELUWE “Upset Minded”.

Wapendwa kuna adui wa Ndoa yako, anayekuonea wivu unapokula Maraha na mpenzi wako, kila wakati anapanga njama namna ya kulihujumu Penzi lenu – naye ni SHETANI. Hata kama ndoa yako haijawahi kupitia migogoro, jua huyu adui anaipigia mahesabu, siku moja utashangaa mambo yamebadilika, Kitanda cha futi sita kitakuwa kama Mahabusu. Mwingine utasikia ansema, mume wangu siku hizi ni USINIGUSE. Hii ndiyo kazi ya Huyu adui, kuleta huzuni sehemu ya Furaha, kama alivyoleta kwa wazazi wetu wa Kale ADAM na HAWA. Ukiona tatizo limeingia, usihangaike kutafuta mchawi au kumuona mwenzio ni Mbaya, wala usitafute kulipa kisasi – Dawa ni kupeleka shitaka kwa Mungu, Mwenye uwezo wa KUMSETA (TO CRUSH) yaani kumharibu Shetani.

Mama mmoja alikuja analia, macho mekundu, nikamuuliza nini kimemsibu, kumbe mume wake anatembea na shoga yake, na mwishowe akaamua kuhamia kabisa. Nilimpa Dawa ambayo hadi sasa anaisifia, Mume amerudi nyumabani. Nilimwambia – Kwanza amsamehe mume wake, kwani kuna adui aliyesababisha hayo yote  – Pili amuombe Mungu Aharibu kazi hizo za Shetani. Baada ya Maombi – Mwanaume kila akienda kucheza MECHI na nyumba ndogo hafanyi kazi, akafikiri amelogwa, akaenda kwa wanganga hadi WAMASAI, nguvu za KI - hazikurudi, akienda kwa mkewe anakuwa na Nguvu kama Simba. Mwishowe akaona hana jinsi, akarudisha majeshi nyumbani, na Mama sasa anakula kwa Raha zake.

 Rafiki usitumie nguvu na akili zako kutatua matatizo ya Ndoa yako, salimisha maisha yako kwa Mungu, halafu Mtwishe yeye Fadhaha zako, ana njia maelfu za kukushindia. Shetani si chochote si lolote, ndiyo maana anafanya kila mbinu kututenga na Mungu, anajua tukiwa na Mungu hana uwezo wa nasi – MUNGU WA AMANI ATAMSETA CHINI YA MIGUU YETU UPESI, (GOD WILL BRUISE SATAN UNDER OUR FEET SHORTLY).

MUNGU ATUANGAZIE NURU YA USO WAKE NA KUTUPATIA AMANI TELE

Ev:  Eliezer Mwangosi.

AGIZO LA KUWAACHA WAZAZI

UJUMBE UNATOKA:  Mwanzo 2:24
Kwa hiyo mwanamume atamwacha Baba yake na Mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja
TAFAKARI:
Kati ya matatizo yanayochangia Ndoa nyingi kutokuwa na AMANI ni swala la Wanandoa kutowaacha wazazi wao. Ni kweli damu ni nzito kuliko maji, lakini Mungu anatoa agizo la wanandoa kuanzisha himaya yao. Magomvi tunayoyashuhudia kati ya – Mawifi, Mama mkwe, wakamwana, Mashemeji na Baadhi ya wanandoa, yanatokana na kutoelewa agizo hili. Agizo la kuwaacha wazazi lina maana kubwa, baadhi ni hizi:

1.    Wanandoa wasianzie maisha kwenye kaya za wazazi wao, yaani wasiishi na Familia za wazazi wao. Wanapaswa kuanzisha himaya yao, yenye uhuru kamili wa maamuzi juu ya maisha yao.

2.    Ndugu wasaidiwe, lakini wasipewe nafasi ya kiutawala, kuna mashemeji wanatoa Amri utafikiri ni nyumbani kwao. Mke ameolewa na mmoja, athaminiwe, mara nyingi akina Dada (Mawifi), wanaona wivu kwa kila kitu anachofanyiwa wifi yao, wanaume wanatakiwa kuwa na Msimamo juu ya wake zao, Mke ni Ubavu na ni mwili mmoja.

3.    Siri za Mke na Mume zisitoke kwenda kwa Ndugu, labda kwa
makubaliano inapobidi. Kuna wanandoa hawatulii, kila jambo lazima liende kwa Ndugu. Mara nyingi Dharau zinaanza kwa kutotunza Siri.

4.    Inapolazimu kukaa na Wazee- mfano. Mama Mkwe, ni wajibu wa mwanamume kumlinda mke wake, mara nyingi akina Mama wakiwa kwa watoto wao wa kiume wanajitwalia Madaraka, na kujiona ni wa muhimu kuliko wakwe zao, atataka apatiwe mahitaji zaidi au sawa na mkwe wake. Wengine wanataka kufanana hadi nguo za Ndani.

5.    Kama mtakaa na Ndugu wa upande wowote, hakikisheni hawaingilii uhuru wenu wa faragha.

6.    Endapo kumetokea kutoelewana kati ya wanandoa, usipeleke mashitaka kwa wazazi wako, peleka mashitaka kwa wazazi wa mwenzio. Wazazi wako mara nyingi hawataona kosa lako, hivyo ni rahisi tatizo kutopata ufumbuzi.

Mawifi, Mashemeji, Akina Mama na Baba Mkwe, na wakamwana – Tafadhalini sana waachieni wanandoa nafasi na Uhuru, hao ni mwili mmoja. Wanandoa msiogope mawimbi yakiwapata, Mungu yupo atawashindia Daima, anao uwezo wa kutuliza DHORUBA.

MUNGU ABARIKI NDOA NA FAMILIA ZETU ILI ZIWE NA FURAHA DAIMA
  
Ev:  Eliezer Mwangosi.

NDOA NA MATUMIZI YA FEDHA

Ujumbe wa Leo unatoka:  1 Timotheo 6:10
Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda FEDHA;  ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani na kujichoma kwa maumivu mengi”
TAFAKARI:a
Kama tunavyoshuhudia, matukio mengi ya kutisha mfano: Mauaji hadi ya Albino, Ujambazi, Ukahaba, Ufisadi, Wizi n.k. huchangiwa na kupenda Fedha. Pia Ndoa nyingi leo zinaathirika na swala hili la Pesa, leo kwa ufupi tunaangalia njia za kutatua matatizo ya NDOA yanayotokana na fedha.

1.   Ubinafsi katika Vipato: Hili ni tatizo kubwa, kwenye ndoa hakuna neno changu, kuna neno CHETU, hivyo vipato vinatakiwa viwekwe wazi, ili vipangiwe matumizi kwa pamoja. Mifumo Dume haitakiwi, na wengine wanasema kipato cha baba ni cha Familia na kipato cha Mama ni Chake Mwenyewe – Huo ni Ubinafsi.

2.   Matumizi ya Fedha yapangwe na wanandoa wote, yakizingatia pia matumizi binafsi “Pocket Money”. Kama mama hana kipato, fedha kiasi itengwe kwa ajili ya matumizi yake binafsi. Kununua vitu vya thamani bila kumshirikisha mwenzio tayari ni tatizo – mwenzio atajua una pesa nyingi umemficha. Moja kwa moja Imani inapotea na wakati wote atafikiri una Mapesa na kuna mambo ya siri unayafanya bila ya yeye kujua.

3.   Familia iwe na Vipaumbele, hapa inahitajika hekima, make watu wanatofautiana mitazamo: Mwanaume utakuta anapenda music system ya Kisasa wakati Mama anataka Jiko kubwa la gesi, na fedha haitoshi, hilo ni tatizo tayari.

4.   Kutokana na hali ya maisha kwa wengi kuwa Ngumu na Vipato kuwa vidogo – inahitajika Busara na kuwa na KIASI juu ya kupanga matumizi. Inahitaji Upendo wa Kweli ambao utawaunganisha nia zenu kuwa kitu kimoja. Amueni kuishi kulingana na Kipato chenu.

Ushauri kwa wanaume: Acheni kutumia fedha ovyo kwa mambo ya Starehe huku akina Mama wakibeba mizigo mizito ya kuhangaika na familia, ulevi na machangudoa ni sumu ya Maisha ya Ndoa.
Ushauri kwa wanawake wenye Vipato Vikubwa kuzidi waume zao: Kuweni na Busara, wapeni waume zenu heshima ya kuwa Baba wa Familia, kuweni na kiasi katika kuvaa, sio kila toleo kitenge uwe nalo.

MUNGU ALINDE FAMILIA ZETU NA KUTUPATIA UPENDO, AMANI NA FURAHA KATIKA MAISHA YETU YOTE.

Ev. Eliezer Mwangosi