Thursday, December 29, 2011

MALEZI YA WATOTO

UJUMBE WA LEO:  Mithali 22:6
“Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee”
tAFAKARI:
Kuna visa vingi tunavishuhudia juu ya tabia za Watoto wa kizazi cha leo, siku moja tulikuta mwalimu anaendesha Kesi kati ya Mtoto wa kiume wa darasa la tatu aliyekuwa amembaka mtoto wa kike. Alivyoulizwa mambo hayo ameyajulia wapi, akadai alifundishwa na Dada yake mlezi (House Girl). Kumbe tangia alipokuwa mtoto mdogo House Girl alikuwa akimfanyia mchezo wa kukidhi haja yake ya Ngono. Wazazi wengi wanalia juu ya tabia za watoto wao kuharibika, mara nyingi tunasikia “Heri kutozaa kuliko kuzaa mtoto wa tabia hii” Kama watoto wako hivyo! unategemea kuwa na Vijana wa namna Gani na hatimaye wazee wa namna gani?.

Kulingana na mfumo wa maisha tunaoishi, ni ndoto za mwenda wazimu kuwa na Jamii yenye maadili kwa sababu:
1.    Wazazi hawana Muda na watoto wao, Mfanyakazi ndiye mlezi, hivyo watoto wanarithi tabia ya House girls. Mama na Baba hawana muda wa kukaa na watoto, sanasana weekend, nazo utakuta kila mtu yuko busy na shughuli za nyumbani.
2.    Walezi wengine wa watoto ni TV, watoto wanaharibika kwa sababu, muda mwingi wako huru kuangalia TV, kwa sababu wazazi muda mwingi hawako nyumbani. Na zaidi utakuta Mdada wa kazi yuko huru kujiwekea Picha zozote, ambazo athari yake ni kubwa kwake mwenyewe na watoto.
3.    Wazazi wengi wa siku hizi hawako makini na mambo wanayoyafanya mbele za watoto. Watoto wengi utaona wanafanya  mchezo wa Baba na Mama, Baba juu na Mama chini, wanaona wapi? Kama sio mtindo wa kulala na vitoto, utafikiri watoto wamelala kumbe wanasikilizia, huku wakiinua shuka kuchungulia. Wengine vyumba vyao havina Siri, chumba cha pili kikiwa cha watoto, Faragha ikianza tu, watoto chumba cha pili ni shida tupu, unafikiri hao watoto au vijana kesho watafanya nini?
4.    Watoto hawapati Muda mzuri wa kujifunza neno la Mungu, ambalo ndilo linaweza kuwahekimisha. Neno la Mungu linasema “Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, bali Wapumbavu hudharau hekima na Adabu” Mithali 1:7.

Wapendwa, pamoja na Maisha haya, tunawajibika kulea watoto, Mtoto anatakiwa kurihi tabia ya Mama, Ndiye mwalimu wake mkuu, Akili ya mtoto inakuwa tupu anapozaliwa, anategemea akili ijazwe na mambo anayosikia na anayoona kila mara. Je Mtoto wako akili yake inajazwa na Maneno na Matendo ya NANI? Hiyo ndiyo tabia yake ya Baadaye. Matusi na Maneno yasiofaa hayatakiwi mbele za watoto.

MUNGU ABARIKI FAMILIA ZETU NA KUTUPATIA BUSARA ZA NAMNA YA KULEA KWA AJILI YA MAFANIKIO YA BAADAYE 

Ev:  Eliezer Mwangosi

No comments:

Post a Comment