Sunday, February 12, 2012

MUME MWEMA

Neno la leo linatoka: 1Petro 3:7
“Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa AKILI; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe”
TAFAKARI:
Kwa asilimia kubwa matatizo yanayotokea katika ndoa chanzo chake ni mwanaume kutojua kuishi kwa akili na Mke wake. Ni kweli kuna wanawake wajinga ambao biblia inasema wanavunja nyumba zao kwa mikono yao wenyewe, pamoja na hayo kama mwanaume ataomba Mungu ampatie Hekima au akili Ndoa inadumu. Kumbuka kila unalotenda kwa mwenzio linazaa tendo la kutendewa likiwa baya au jema. Tatizo likitokea katika ndoa, kaeni chini mtafute chanzo cha tatizo, Mume ana sehemu ya kutumia akili aliyopewa na Mungu kurudisha mahusiano. Hebu tuangalie baadhi tu ya mambo anayotakiwa mwanaume kumtendea mkewe:

MUME AMHESHIMU MKE WAKE: Kuna wanaume wanadharau wake zao, utakuta mke anatukanwa, kupigwa, anakosolewa mbele ya watoto au hata mbele ya watu kama house girl. Mara ngapi tunasikia wanaume wakigomba “Mama Fulani chakula gani hiki mbona ugali haujaiva vizuri?”, lawama hizo mbele za watu au mabinti wa kazi – ni kumuaibisha mkeo, na kwake ni tatizo kubwa. Mke ni tofauti kabisa na watoto au wasichana wa kazi, anatakiwa kupewa Heshima, huyo ni mwenzi wako na mshauri wako. Kufanya Mapenzi na wanawake wengine ni kumdhalilisha mkeo na kwa sababu mapenzi hayagawanyiki lazima matatizo yataanza.

MUME AMJALI NA KUONYESHA UPENDO KWA MKE: Mwanamke ana hisia kali za mahusiano, anabadilika kulingana na anavyotendewa, wakati mwingine wanakuwa kama watoto, unaweza kumdanganya hata kwa kitu kidogo ili mradi kiashirie kumpenda. Siku moja jaribu kununua Pipi, halafu mwambie “sweet” au “Darling” nimekuletea zawadi kubwa, twende nikakupe chumbani, halafu toa pipi huku ukimtazama usoni, utashangaa yatayotokea. Onyesha kuwa unamjali, unamthamini, unampenda na unafurahia ukiwa nae. Hata kama ana kazi yake, Mnunulie nguo rasmi kama zawadi. Neno Pole Mpenzi, Samahani, Umependeza n.k. yana maana sana kwa Mwanamke. Mume awe na muda wa kuongea na Mke wake, kushinda kwenye Mabaa hadi usiku, kuwa busy na TV au Kompyuta muda wa usiku ni tatizo kwa mwanamke. Wanaume wengi wanacheka na kupiga porojo na wanawake wengine maofisini, lakini akifika nyumbani utafikiri ameambiwa yuko mahakamani penye amri ya usipige kelele.  

MUME NI KICHWA CHA NYUMBA: Tangia mwamzo Majukumu ya kutunza familia ni ya Baba, mwanamke ni msaidizi, siku hizi mambo yamegeuka, akina mama ndio wanaachiwa mizigo ya kulea familia, Mke akiwa na kazi au biashara ndio usiseme, Nguo za watoto, chakula, ada n.k. yote anaachiwa Mama. Baba hakikisha unaacha fedha za kutosha nyumbani, wengi wanapenda chakula kizuri huku wanaacha fedha za fungu moja la mchicha, na wengine wanakula vizuri wakiwa kazini – Supu, Biliani, Pilau mbuzi, Juice – familia nyumbani ni maharage wakibadilisha Mchicha.

MPATIE HAKI YAKE YA NDOA: Ni wajibu wa Mume kumtimizia mkewe hitaji la Ndoa, jambo hili siku hizi limekuwa tatizo kubwa. Wanaume wengi WANABAKA wake zao, kwa maneno rahisi ni kwamba wanafanya tendo la ndoa kutimiza wajibu sio kwa ajili kupeana mapenzi. Utakuta mwanaume anaparamia tu wala hakuna maandalizi, siku nzima wameshinda hawaongei, usiku ukifika ni Amri za Jeshi “SIMAMA JUU, KULIAAAA GEUKA, MGUU PANDE, MWILI LEGEZA” hizo kwa mwanamke ni Karaha au Adha badala ya Raha. Wanaume wengi ni wabinafsi katika swala hilo, wanajali kutimiza haja zao, kuna akina mama hawajawahi kufikishwa mwisho wa Raha, japo kila siku wanatoa huduma. Hili jambo linahitaji elimu ili kila mmoja aone furaha ya Ndoa. Kwa tatizo la kiafya, nitalitolea maelezo katika somo lijalo, hakuna haja ya kuwatajilisha wamasai kwa dawa zao za kutunza heshima ya Ndoa.

MUNGU ABARIKI NDOA ZETU ZIWE NA MWANZO MPYA WENYE FURAHA NA AMANI TELE

Ev:  Eliezer Mwangosi.
0755808077 & 0652571733

No comments:

Post a Comment