Sunday, April 1, 2012

ADUI ANAYETESA FAMILIA


Ujumbe  unatoka:  Mathayo 5:27-28
Mmesikia kwamba imenenwa, USIZINI; lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kutamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.
tAFAKARI:
Wiki mbili zilizopita, Familia mbili ziliingia kwenye misiba ya kusikitisha baada ya Baba wa familia moja na Mama wa familia nyingine kupata ajali ya gari na kufa papohapo wakiwa wanatoka kupeana mapenzi. Mama (marehemu) alikuja likizo, mume na watoto aliwaacha ulaya, na Baba (Marehemu) alikuwa anaishi hapa Dar na familia yake, siku hiyo marehemu hawa walikutana, na wakakubaliana kukumbushia mapenzi waliyokuwa wakipeana wakiwa marafiki kabla ya Ndoa. Shetani hakuwaachia Pumzi, siku hiyohiyo ikawa ya RAHA na mara kugeuka kuwa ya HUZUNI NA MAUTI, “One mistake one Goal”.

Marafiki zangu, kama kuna adui mkubwa anayetesa familia katika vizazi vyote ni Dhambi ya UZINZI, yaani Tendo la Ndoa kati ya watu wawili wasio katika NDOA Halali. Familia nyingi zimesambaratishwa, watoto wanahangaika utafikiri baba kafariki kumbe amesombwa na Kahaba, Familia hazina Furaha wala Amani, Upendo umehamia kwa wenye kunyanyua Chuchu na Makalio ya Mchina. Familia zinapata shida za pesa, huku akina baba wanaitwa mapedeshee, mala ATM, Mabuzi na kila aina ya sifa, bila kusahau Mashugamamiii wanaojituliza kwa vijana.

Kwa bahati mbaya sana, Kila kunapokucha ndivyo Adui huyu mkubwa “ZINAA” anazidi kupata umaarufu katika Jamii, anashabikiwa na kila Mtu, kuanzia watoto hadi vikongwe, maskini hadi wafalme, wapagani hadi kwa manabii na Mitume feki. Ni mara ngapi tumesikia vituko vya kwenye Ma “Guest House” vizito kuibiwa na Machangu Doa, Makanisani wachungaji kula kondoo wao, mashuleni walimu na wanafunzi, na vyuoni ndiyo usiseme, maofisini mabosi na wafanyakazi wao, na zaidi hata kwenye mabasi (daladala) wanavyobanana, unashangaa mwanaume tayariiii (Eti Mfadhaiko). HILO NI PEPO LA NGONO.

Amri ya Saba katika zile Amri kumi inasema “USIZINI” Kutoka 20:14, pamoja na kuhalalishwa na watu wengi, Mungu anasema “Ikimbieni ZINAA. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye ZINAA hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. Au hamjui ya kuwa MWILI wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu akaaye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu” 1Korintho 6:18-20.  Kizazi cha NUHU na Sodoma Mungu aliwaangamiza kwa sababu ya huyu adui Mtesaji na Muuaji “ZINAA”.

Wapendwa tendo la Zinaa ni sawa na Kulamba Sukari iliyotiwa SUMU, na wengi hawajui hilo, hatimaye wanaishia kwenye maisha ya Majuto na Kukata tamaa kama sio kifo, na hatimaye Jehanamu ya Moto. Wengi wanadai huwezi kuishinda Zinaa, ni kweli, hata Yesu alisema “Mimi ni Mzabibu; ninyi ni matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; MAANA PASIPO MIMI NINYI HAMWEZI KUFANYA NENO LO LOTE” Yohana 15:5. Ushindi wa dhambi hii ya Zinaa, ni kwa, kuruhusu Roho Mtakatifu akaye ndani yetu, ambaye anaua chembechembe za Virusi vya Dhambi (Tamaa ya mwili) na Kutupatia tabia ya Mungu ndani ya MIOYO YETU, na huku ndiko kuzaliwa UPYA. 

SWALI limeulizwa; je na wewe imepitiwa na huyu adui anayetesa familia? Jibu kwa asilimia kubwa ni Ndiyo, hata kama wewe hujawahi kuanguka kwenye Zinaa, kwa namna moja au nyingine umeyaonja madhara yake, kupitia familia tunazoishi nazo. Wito wangu ni huu, wote walioathirika na jambo hili, Mlango bado uko wazi, Rehema za Mungu bado zipo kutusaidia Kushinda na Kutuvusha salama.

BARAKA ZA BWANA ZAKAAMBATANE NANYI WOTE DAIMA – NAWATAKIA SIKU NJEMA

Ev:  Eliezer Mwangosi.