“Muwe na HASIRA, ila msitende dhambi; Jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka”
TAFAKARI:
Asilimia kubwa ya NDOA za siku hizi hazina AMANI, utasikia mama anasema heri nisingeolewa, na wakati mwingine Baba anafikiri alikosea, huenda huyo mwanamke halikuwa chaguo sahihi. Wanasahau kuwa wakati wa uchumba na hatimaye “honey moon” (Fungate), walikuwa wakipakatana wakilishana na kunyweshana Juice. Lakini leo watu wanalala huku wanaomba usiku uishe haraka.
Leo tunatafakari juu ya HASIRA na Kuwa na machungu moyoni, Kuna watu wanahasira za Kijinga, utakuta mtu amefura hawezi hata kuongea. Lakini ukifuatilia utakuta KOSA ni dogo, mfano: Mwanamke anamuona mume wake anacheka na mdada anayefanya naye kazi. Moja kwa moja wazo linamtuma kuwa anaibiwa, Mara mama anaanza kununa, inafika usiku Mama anapanda kitandani na NGUO utafikiri ameambiwa ajiandae kukimbiza mwizi usiku. Na mwanaume akiona adhabu inazidi, siku ya kwanza, ya pili, ya tatu, wiki - anaanza kuzungusha macho barabarani utafikiri “WIPER” za Isuzu. Unashangaa Mama anaanza kuvaa kanga za Mafumbo “Utazunguka kila Bucha Nyama ni ileile” na utakuta Baba wala hana habari ya Kusoma maneno ya Kanga. Mwisho wa yote NDOA inaishia kuwa Jera ndogo ambayo, Upendo, Furaha na Amani vinabaki kuwa historia.
Wapendwa, hasa wenye ndoa changa, jueni kuwa, Ndoa ni Muungano wa watu wawili waliodhaifu, walioazimia kuishi wakichukuliana na kusaidiana. Tatizo sio kukosewa au kukwazwa, shida kubwa ni namna ya kuchukuliana hasa mwenzio anapokukosea. Kumbuka mwanadamu yeyote sio mkamilifu “SIO MALAIKA”, hivyo kukoseana lazima kutatokea, na SHETANI anaitumia hali ya kukoseana vizuri, atakuletea hisia mbaya na kukujaza hasira na Machungu Moyoni ambayo madhara yake ni SUMU YA NDOA. Katika hali zozote unapoona umekosewa, omba hekima kwa MUNGU atakupatia njia nzuri ya kulitatua tatizo kwa AMANI, waswahili walisema “HASIRA - HASARA”. Mungu anasema "Hasira hukaa kufuani mwa wapumbavu" Mhubiri 7:9
MUNGU ATAWALE NDOA NA FAMILIA ZETU – NAWATAKIA SIKU NJEMA
Ev. Eliezer Mwangosi
No comments:
Post a Comment