“Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu”
TAFAKARI:
Kama kuna bidhaa adimu katika maisha ya siku hizi, ni HESHIMA KATIKA NDOA. Wana ndoa asilimia kubwa hawaheshimiani, lakini pia hata watu wa nje hawaheshimu Ndoa za wenzao.
Utasikia matusi ya nguoni yakirushwa kati ya wanandoa mbele za watoto, magomvi ya usiku yasiyokoma, kunyanyasana, dharau, maneno ya mikato, kununiana n.k. yote hayo ni kukosa heshima katika ndoa.
Mawifi, mashemeji, akina mama mkwe n.k. tunashuhudia wakianzisha tafrani katika ndoa za ndugu zao. Bila kuwasahau wanaowasha mapenzi kwa waume au wake za watu. Hayo yote ni kuvunja heshima ya ndoa. Mithali 5:15 inasema “Unywe maji ya Birika lako Mwenyewe”. Uliona wapi watu wanapokezana vijiko wakati wa kula? Huo sio ustaarabu na kukosa HESHIMA.
Sehemu nyingine inayopaswa heshima ni chumbani, sehemu pekee ya kupumzisha akili na kupata furaha ni wakati wa faragha. Wapendwa leo kuna kesi nyingi na matatizo mengi ya wanandoa, hata magonjwa, yanayotokana hapo chumbani. Wengi vyumba vyao vimegeuka kuwa KARAHA, ni amri kama jeshini, ndio maana hata madereva wa magari wanalazimika kwenda Shule, angalia madereva taxi wengi wako “very rough” na gari zao hazidumu.
Pia sharti wanandoa wakumbuke kuwa kila kiungo cha mwili kiliumbwa kwa kazi maalumu, ndio maana hatujawahi kuona wanyama wanafanya tendo la ndoa kinyume na maumbile, mambo hayo athari zake ni kubwa. Hebu, UPENDO NA AMANI vitawale katika viwanja vya FARAGHA.
NAWATAKIA SIKU NJEMA YENYE AMANI NA MAFANIKIO TELE
Na: Eliezer Mwangosi
No comments:
Post a Comment