Monday, January 9, 2012

KUWAACHA WAZAZI NA KUWA MWILI MMOJA

NENO LA LEO:  Mwanzo 2:24
Kwa hiyo mwanamume atamwacha Baba yake na Mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja
TAFAKARI:
Kati ya matatizo yanayochangia Ndoa nyingi kutokuwa na AMANI ni swala la Wanandoa kutowaacha wazazi wao. Ni kweli damu ni nzito kuliko maji, lakini Mungu anatoa agizo la wanandoa kuanzisha himaya yao. Magomvi tunayoyashuhudia kati ya – Mawifi, Mama mkwe, wakamwana, Mashemeji na Baadhi ya wanandoa, yanatokana na kutoelewa agizo hili. Agizo la kuwaacha wazazi lina maana kubwa, baadhi ni hizi:

1.    Wanandoa wasianzie maisha kwenye kaya za wazazi wao, yaani wasiishi na Familia za wazazi wao. Wanapaswa kuanzisha himaya yao, yenye uhuru kamili wa maamuzi juu ya maisha yao.

2.    Ndugu wasaidiwe, lakini wasipewe nafasi ya kiutawala, kuna mashemeji wanatoa Amri utafikiri ni nyumbani kwao. Mke ameolewa na mmoja, athaminiwe, mara nyingi akina Dada (Mawifi), wanaona wivu kwa kila kitu anachofanyiwa wifi yao, wanaume wanatakiwa kuwa na Msimamo juu ya wake zao, Mke ni Ubavu na ni mwili mmoja.

3.    Siri za Mke na Mume zisitoke kwenda kwa Ndugu, labda kwa makubaliano inapobidi. Kuna wanandoa hawatulii, kila jambo lazima liende kwa Ndugu. Mara nyingi Dharau zinaanza kwa kutotunza Siri.

4.    Inapolazimu kukaa na Wazee- mfano. Mama Mkwe, ni wajibu wa mwanamume kumlinda mke wake, mara nyingi akina Mama wakiwa kwa watoto wao wa kiume wanajitwalia Madaraka, na kujiona ni wa muhimu kuliko wakwe zao, atataka apatiwe mahitaji zaidi au sawa na mkwe wake. Wengine wanataka kufanana hadi nguo za Ndani.

5.    Kama mtakaa na Ndugu wa upande wowote, hakikisheni hawaingilii uhuru wenu wa faragha.

6.    Endapo kumetokea kutoelewana kati ya wanandoa, usipeleke mashitaka kwa wazazi wako, peleka mashitaka kwa wazazi wa mwenzio. Wazazi wako mara nyingi hawataona kosa lako, hivyo ni rahisi tatizo kutopata ufumbuzi.
Mawifi, Mashemeji, Akina Mama na Baba Mkwe, na wakamwana – Tafadhalini sana waachieni wanandoa nafasi na Uhuru, hao ni mwili mmoja. Wanandoa msiogope mawimbi yakiwapata, Mungu yupo atawashindia Daima, anao uwezo wa kutuliza DHORUBA.

MUNGU ABARIKI NDOA NA FAMILIA ZETU ILI ZIWE NA FURAHA DAIMA
  
Ev:  Eliezer Mwangosi.

No comments:

Post a Comment