Ujumbe wa Leo unatoka: 1 Timotheo 6:10
“Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda FEDHA; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani na kujichoma kwa maumivu mengi”
TAFAKARI:a
Kama tunavyoshuhudia, matukio mengi ya kutisha mfano: Mauaji hadi ya Albino, Ujambazi, Ukahaba, Ufisadi, Wizi n.k. huchangiwa na kupenda Fedha. Pia Ndoa nyingi leo zinaathirika na swala hili la Pesa, leo kwa ufupi tunaangalia njia za kutatua matatizo ya NDOA yanayotokana na fedha.
1. Ubinafsi katika Vipato: Hili ni tatizo kubwa, kwenye ndoa hakuna neno changu, kuna neno CHETU, hivyo vipato vinatakiwa viwekwe wazi, ili vipangiwe matumizi kwa pamoja. Mifumo Dume haitakiwi, na wengine wanasema kipato cha baba ni cha Familia na kipato cha Mama ni Chake Mwenyewe – Huo ni Ubinafsi.
2. Matumizi ya Fedha yapangwe na wanandoa wote, yakizingatia pia matumizi binafsi “Pocket Money”. Kama mama hana kipato, fedha kiasi itengwe kwa ajili ya matumizi yake binafsi. Kununua vitu vya thamani bila kumshirikisha mwenzio tayari ni tatizo – mwenzio atajua una pesa nyingi umemficha. Moja kwa moja Imani inapotea na wakati wote atafikiri una Mapesa na kuna mambo ya siri unayafanya bila ya yeye kujua.
3. Familia iwe na Vipaumbele, hapa inahitajika hekima, make watu wanatofautiana mitazamo: Mwanaume utakuta anapenda music system ya Kisasa wakati Mama anataka Jiko kubwa la gesi, na fedha haitoshi, hilo ni tatizo tayari.
4. Kutokana na hali ya maisha kwa wengi kuwa Ngumu na Vipato kuwa vidogo – inahitajika Busara na kuwa na KIASI juu ya kupanga matumizi. Inahitaji Upendo wa Kweli ambao utawaunganisha nia zenu kuwa kitu kimoja. Amueni kuishi kulingana na Kipato chenu.
Ushauri kwa wanaume: Acheni kutumia fedha ovyo kwa mambo ya Starehe huku akina Mama wakibeba mizigo mizito ya kuhangaika na familia, ulevi na machangudoa ni sumu ya Maisha ya Ndoa.
Ushauri kwa wanawake wenye Vipato Vikubwa kuzidi waume zao: Kuweni na Busara, wapeni waume zenu heshima ya kuwa Baba wa Familia, kuweni na kiasi katika kuvaa, sio kila toleo kitenge uwe nalo.
MUNGU ALINDE FAMILIA ZETU NA KUTUPATIA UPENDO, AMANI NA FURAHA KATIKA MAISHA YETU YOTE.
Ev. Eliezer Mwangosi
No comments:
Post a Comment